MBOZI. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, George Musyani amewataka watendaji kata na vijiji kusimamia ukusanyaji wa mapato katika maeneo yao ili kuinua mapato ya halmashauri hiyo.
Musyani ametoa wito huo Alhamisi Februari 2, 2023 wakati wa mkutano wa Baraza kamili la Madiwani wakiwasilisha taarifa za kata katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi.
Amesema kuwa ukusanyaji mzuri wa mapato ndio unaopelekea kuleta miradi mbalimbali katika maeneo ya wananchi.
"Bila pesa hakuna kitakacho fanyika, hakikisheni mnawaelimisha wananchi kila nyama inayokaguliwa inakuwa na kibandiko, wasile nyama ambazo hazijakaguliwa" amesema
Amewataka watendaji hao kusoma mapato na matumizi mara kwa mara ili wananchi kujua ya mapato katika maeneo yao.
"Hakikisheni mnasoma mapato na matumizi katika vijiji vyenu na mitaa yenu kwani bila kufanya hivyo mnakuwa hamuwatendei haki wananchi" amesema mwenyekiti huyo wa halmashauri na kuongeza;
"Kwa upande wa kusimamia miradi mtendaji ukisimamia vizuri katika kata yako au kijiji chako inaonekana serikali inafanya kazi vizuri"
Pia, amewataka watendaji hao kuhakikisha watoto wenye umri wa kwenda shule wote waandikishwe na wanaende shuleni.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo amekumbusha watendaji hao kusimamia kikamilifu utolewaji wa chakula mashuleni.
Mbozi
Anuani: 3
Simu: 025-2580272
Simu ya kiganjani:
Barua pepe: ded@mbozidc.go.tz
Hati Miliki 2017 Halmashauri ya Wilaya-Mbozi. Haki zote zimehifadhiwa