Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Mhe. Hamadi Mbega, amefanya ziara ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika Kata ya Ipunga huku akihamasisha ushirikiano baina ya Serikali na jamii katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mbega alitembelea Shule ya Msingi Ipunga na kujionea hali ya miundombinu ya shule pamoja na changamoto zinazowakumba walimu na wanafunzi huku akiwasisitiza walimu kuendelea kutoa elimu bora.
Pia, alitembelea Zahanati ya Kata ya Ipunga, ambapo alikagua utoaji wa huduma za afya kwa wananchi akisisitiza umuhimu wa kuboresha huduma hizo.
DC Mbega ambaye alishiriki mkutano mkuu wa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Kata ya Ipunga aliwataka wajumbe hao kushirikiana kwa karibu na serikali katika kutatua changamoto za kijamii na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi na uzalendo mkubwa.
Aidha, amewahimiza wananchi kufanya kazi kwa bidii katika shughuli zao mbalimbali za kiuchumi kama kilimo, ufugaji, na biashara.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mbega aliwasisitiza wananchi kuyasemea mazuri yanayofanywa na Serikali, ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama barabara, huduma za afya, na elimu. Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali na wananchi ni msingi wa maendeleo endelevu.
Mhe. Mbega aliwaeleza wananchi umuhimu wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu pamoja na kutoa rai kwa wananchi kudumisha mshikamano na amani katika jamii, akieleza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila ushirikiano wa kijamii na utulivu.
Ametoa wito kwa viongozi wa vijiji na kata kuhakikisha wanashirikiana na wananchi kuibua miradi mipya ya maendeleo na kuhakikisha rasilimali za umma zinatumiwa kwa manufaa ya jamii yote akieleza kuwa Serikali ya Wilaya itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo kwa uadilifu na kuhakikisha changamoto zao zinashughulikiwa kwa wakati.
Mbozi
Anuani: 3
Simu: 025-2580272
Simu ya kiganjani:
Barua pepe: ded@mbozidc.go.tz
Hati Miliki 2017 Halmashauri ya Wilaya-Mbozi. Haki zote zimehifadhiwa