Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Mhe. Hamad Mbega amesisitiza uimarishaji na usimamizi wa vyama vya ushirika ili kuleta tija kwa wakulima na wananchi wa wilaya hiyo na Mkoa wa Songwe kwa ujumla
Mhe. Mbega ametoa maagizo hayo leo Jumanne Machi 18, 2025 katika mkutano mkuu wa vyama vya Ushirika uliofanyika mjini Vwawa.
Mhe. Mbega ameagiza vyama vyote vya ushirika kuhakikisha vinahuisha na kuimarisha mifumo yao ya ndani lengo likiwa ni kuboresha uwazi na uwajibikaji unaowezesha vyama hivyo kufanya kazi kwa ufanisi na kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa wanachama wake.
Pia, Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza vyama vyote vya ushirika viungane na Chama Kikuu cha Ushirika (SORECU) ili kuimarisha mshikamano na kuwezesha usimamizi bora wa shughuli za vyama vya ushirika katika ngazi za wilaya.
Katika Mkutano huo Mhe. Mbega amevisisitiza vyama hivyo kufanya maandalizi ya mapema kwa ajili ya ukusanyaji wa mazao ya ufuta, ambapo amesema maandalizi ya mapema ni msingi wa mafanikio katika msimu wa kilimo.
"Ushirika ni mali ya wananchi, wanachama wa vyama vya ushirika wanapaswa kutumia fursa hiyo kuleta manufaa kwa jamii zao, viongozi wa vyama vya ushirika hakikisheni mnanatoa huduma bora kwa wanachama wenu ili kukuza uaminifu na ushirikiano wa kweli" amesema
Katika hotuba yake, Mkuu huyo wa Wilaya ameeleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na vyama vya ushirika ili kuhakikisha kuwa rasilimali zinazotokana na kilimo zinatumika kwa manufaa ya watu wote.
"Maendeleo ya kilimo yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya serikali, vyama vya ushirika, na wakulima".
Ametoa mwito kwa viongozi wa vyama hivyo kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha kuwa wanazingatia maslahi ya wanachama wao
Mbozi
Anuani: 3
Simu: 025-2580272
Simu ya kiganjani:
Barua pepe: ded@mbozidc.go.tz
Hati Miliki 2017 Halmashauri ya Wilaya-Mbozi. Haki zote zimehifadhiwa