Wilaya ya Mbozi ni wilaya moja wapo katika wilaya 5 za mkoa wa Songwe. Wilaya hiyo ilianzishwa rasmi tarehe 27/1/ 1974 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Julius Kambarage Nyerere .
Asili ya jina ‘’Mbozi’’ linatokana na na dawa za asili zilizotengenezwa na majani ya miti yanayochumwa kisha kutwangwa kwenye kinu na kuongezewa maji kidogo kisha kuchujwa na kupewa mgonjwa, wanyiha huita dawa hiyo “Mbozyo” ambapo wazungu walishindwa kutamka neno Mbozyo wakatamka “Mbozi”.
Wilaya ya Mbozi iko upande wa Kusini Magharibi mwa Mkoa wa Mbeya, kati ya Latitudo 80 na 90 12’ kusini mwa Ikweta na Longitudo 320 7’ 30’’ na 330 2’ 0’’ Mashariki mwa Greenwich Meridian.
Wilaya ya Mbozi inapakana na wilaya ya Mbeya kwa upande wake wa Mashariki, Wilaya ya Ileje upande wa kusini, wilaya ya Momba upande wake wa Magharibi na wilaya ya Songwe upande wa Kaskazini.
Migawanyiko ya Eneo na Utawala.
Wilaya inachukua jumla ya eneo la kilomita za mraba 3,404 (Ha 340,400) zilizoainishwa kama:-
i. Ardhi ya kilimo …… 255,300 Ha (75%)
ii. Misitu ya hifadhi ……….....34,040 Ha (10%)
iii. Makazi na matumizi mengine .... 44,252 Ha (13%)
iv. Eneo Lililofunikwa na maji ………………… 6,808 Ha (2%)
Jumla ………………………………………. 340,400 Ha
Wilaya imegawanywa katika Tarafa 4, Kata 29 Vijiji 121 na Vitongoji 665 . Wilaya ya Mbozi ina majimbo mawili ya uchaguzi ambayo ni Jimbo la Vwawa na Jimbo la Vwawa.
Hali ya hewa
Wilaya ya Mbozi iko kati ya mita 1,400 – 2,750 kutoka usawa wa bahari. Kwa wastani hupata mvua kati ya 1350 mm na 1550 mm kwa mwaka; wakati halijoto ni kati ya 200C hadi 280C.
Iko ndani ya ukanda wa nyanda za juu, topografia yake ina sifa ya vilima kadhaa vyenye mito na mabonde yanayofaa kwa shughuli za umwagiliaji .
Katika ukanda huo, kuna aina tatu za udongo nazo ni: udongo wa volkano, udongo wa mfinyanzi wenye mchanganyiko mzuri wa mchanga na tifutifu.
Hali ya hewa yake ina sifa ya joto la wastani na mvua nyingi, kutokana na sifa hizi mazao makuu yanayolimwa katika ukanda huu ni kahawa, mahindi, maharagwe, viazi mviringo, karanga na ndizi vilevile kwa kiwango kidogo viazi vitamu
Idadi ya watu
Kwa mujibu wa sensa ya watu ya mwaka 2022, wilaya ya Mbozi ina wakazi 510,599 ambapo wanaume ni 241,636 na wanawake ni 268,963
Usambazaji kwa Eneo.
Mgawanyo wa watu katika Wilaya unachangiwa kwa kiasi kikubwa na rutuba ya ardhi, hali ya hewa na upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi.
Kundi la kikabila.
Katika wilaya ya Mbozi kabila kubwa ni Wanyiha ambao wanachukua zaidi ya 50% ya watu wote. Makabila mengine ni Wanyamwanga, Wanda, Wanyakyusa, Ndali, Lambya, Malila.
Mbozi
Anuani: 3
Simu: 025-2580272
Simu ya kiganjani:
Barua pepe: ded@mbozidc.go.tz
Hati Miliki 2017 Halmashauri ya Wilaya-Mbozi. Haki zote zimehifadhiwa