Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega amewataka vijana kutotumia fedha wanazokopeshwa na Halmashauri kuchezea kamari maarufu kubeti badala yake wazitumie kwa shughuli walizopanga ili fedha hizo ziweze kuwainua kiuchumi.
DC Mbega ametoa agizo hilo leo Marchi 5, 2025 wakati akiongea katika hafla ya utoaji mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, ambapo zaidi ya Tsh1.298 Bilioni zimetolewa.
Pia, amewataka wanawake kutotumia fedha hizo wanazokopeshwa kwenda kulipia mikopo ya kausha damu wanayodaiwa.
"Msitumie mikopo hii kwa malengo yasiyokusudiwa, mikopo hii mnapewa ili kujinufaisha kiuchumi lakini sio kwa malengo mengine. Vijana msitumie mikopo hii kwaajili ya kubeti au kucheza kamari, mnapewa pikipiki msizitumie kubebea magendo au mkaa. Pia wanawake msitumie fedha hizi kulipa mikopo ya kausha damu" amesema.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, George Musyani amewaasa vijana kuacha tabia ya kutelekeza familia baada ya kupata fedha.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Abdallah Nandonde amewasisitiza wanufaika hao kutotoa kiasi chochote kulipa maofisa waliowasaidia kama fadhila kwa kuwa mikopo hiyo ni haki yao.
Mbozi
Anuani: 3
Simu: 025-2580272
Simu ya kiganjani:
Barua pepe: ded@mbozidc.go.tz
Hati Miliki 2017 Halmashauri ya Wilaya-Mbozi. Haki zote zimehifadhiwa