Songwe . Ili kutokomeza utapiamlo na udumavu kwa watoto katika Mkoa wa Songwe, viongozi na wadau wa mkoa huo wamefikia maazimio yatakayowezesha kuwasaidia wananchi kutatua hali hiyo huku wakisisitiza kuzingatia lishe bora.
Maazimio hayo yamefikiwa leo Jumanne Julai 25, 2023 wakati wa kikao cha tathimini ya viashiria vya mkataba wa lishe wa awamu ya pili ngazi ya mkoa kuanzia Julai 2022 hadi Juni 2023 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe.
Katika kikao hicho ambacho kiliongoziwa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk Francis Michael kilihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo, RMO, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, makatibu tawala wa wilaya za mkoa huo pamoja na maofisa lishe.
Akizungumzia kuhusu kikao hicho na maazimio waliyofikia wadau hao, Mkuu wa Mkoa huo, Dk Francis Michael amesema kuwa kikao hicho kilikuwa cha tathimini na wamefikia maazimio ambayo yatasaidia kuwezesha mkoa kusonga mbele katika suala la kuzingatia lishe bora.
“Leo kama mkoa tulikuwa na kikao cha tathimini ya mkataba wa lishe ambao ulisainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan mwaka jana. Lengo kubwa la vikao hivi ni kwamba taifa linalenga kuhakikisha kwamba lishe inazingatiwa kwa mtoto tangu akiwa tumbioni kwa mama yeke ili kupata kizazi au wananchi wenye afya na akili ya mwili iliyobora” amesema
Amesema kuwa tathimini inaonyesha kuwa mkoa huo uko vizuri kwenye viashiria vinavyozingatiwa katika suala la lishe ambapo upo zaidi ya asilimia 50.
“Tumekaa leo na wadau na tumeongea. Kimsingi mkoa wetu wa Songwe tuko vizuri kwa sababu katika viashiria vyote ambavyo vinakuwa vianzingatiwa kwenye suala la lishe kwa watoto na kwa watu kwa ujumla tuko asilimia zaidi ya 50” amesema
Akitaja baadhi ya maazimio yaliyofikiwa katika kikao hicho, Dk Michael amebainisha“Tumefikia maazimio na katika maazimio ya kikao chetu tumeona kuwa ni lazima wakuu wa wilaya wahakikishe vikao vya tathimini ya masuala ya lishe vikaliwe kila robo mwaka”
“Pia kila halmashauri itenge fedha kutoka katika mapato ya ndani ili kuhakikisha kuwa mikakati inayopangwa inafikiwa ili hata tathimini ikifanywa tusije tukawa tuko chini na kuhakikisha fedha zinazopangwa zinatoka kwa wakati” ameeleza
Mkuu huyo wa Mkoa ametaja azimio linghine linaloweza kusaidia mkoa huo kuzingatia lishe bora kuwa ni pamoja na halmashauri kuhakikisha zinatoa elimu kwa wananchi hadi ngazi za vijijini.
“Tumekubaliana halmashauri kuhakikisha elimu ya lishe inatolewa kwa wananchi mpaka vijijini” amesema
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa ameeleza kuwa wadau hao kwa pamoja wameazimia kila halmashauri kuhakikisha chakula kinatolewa kwa wanafunzi shuleni.
“Lakini tumeazimia mashuleni kuhakikisha vyakula vinatolewa vyenye virutubisho na madini lishe” amebainisha Mkuu huyo wa Mkoa.
Tafiti kufanyika kila wilaya
Akizungumzia umuhimu wa kufanyika utafiti, Dk Michael amesema kuwa ili kufanya tathimini nzuri ni lazima kila Halmashauri kufanya tafiti mbalimbali kujua hali halisi ya hali ya lishe katika halmashauri za mkoa huo.
“Tulizungumzia suala la tafiti kwa sababu ili tujipime kuwa tuko wapi na tumefikia wapi ni lazima tufanye tafiti na ukifanya tafiti matokeo ya tafiti ndio yatakupa picha kamili ya utekelezaji wa kile mnachokipanga kimefanyika kwa namna gani” amesema
Dk Michael amesema kuwa wametoa maelekezo kwa kila wilaya kufanyika tafiti mbalilimbali ambapo matokeo yatapelekwa katika vikao vya tathimini katika mkoa huo.
“Tumekubaliana na halmashauri zitatenga fedha ili tafiti zifanyike na matokeo yake yataletwa kwenye vikao vya tathimini ya masuala ya lishe katika mkoa” amesema
Kuongeza nguvu kwa maofisa lishe
Ili kuongeza nguvu katika utoaji elimu na hamasa ya kuzingatia lishe bora, Dk Michael amesema kuwa wamekubaliana kuajiri wataalamu wa lishe wa muda ambao watasaidia kutatua changamoto hiyo.
Amesema kuwa suala la uhaba wa maafisa lishe wamelizungumzia hilo na kila halmashauri iajiri wataalamu hao kwa mikataba.
“Ni kweli maofisa lishe hawatoshi na Serikali imeshaliona hilo lakini tumekubaliana kuwa kila halmashauri itawaajiri kwa mikataba ya muda mfupi ili tuwe na watu wa kufanya hizo tafiti na kutoa elimu kwa wananchi” amesisitiza.
Rai kwa wananchi
Dk Michael ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe kuhifadhi chakula baada ya kuvuna badala ya kuuza mazao yote.
“Niwaase wananchi wa Mkoa wa Songwe, wanapolima chakula wasikiuze chote na tatizo ni kwamba wengine wanauzia shambani” amesema
Amesema kuwa wananchi wanapovuna wanatakiwa wahifadhi chakula lakini wanapouza wahifadhi fedha kwaajili ya kununulia vyakula vingine.
“Wanatakiwa wanakula chakula chenye lishe ili watoto waweze kula chakula bora kuepuka udumavu na utapiamlo kwa watoto” amesema
Mbozi
Anuani: 3
Simu: 025-2580272
Simu ya kiganjani:
Barua pepe: ded@mbozidc.go.tz
Hati Miliki 2017 Halmashauri ya Wilaya-Mbozi. Haki zote zimehifadhiwa