Wazazi na walezi mkoa wa Songwe wametakiwa kuchukua tahadhari kwa watoto wao kwa kuwapeleka kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio kutokana na ugonjwa huo kutokuwa na tiba.
Pia, wametakiwa kuondoa dhana potofu kuwa chanjo hiyo ina athari kwa binadamu kwa kuwa taarifa hizo hazina ukweli kwani chanjo hiyo ni salama na haina madhara yoyote huku wanahabari wakitakiwa kutoa taarifa sahihi zenye kuhamasisha umuhimu wa chanjo hiyo katika jamii.
Akizungumza wakati wa mafunzo kwa wanahabari wa Mkoa wa Songwe yaliyofanyika leo Jumamosi Septemba 16, 2023 na Afisa Uelimishaji kutoka Wizara ya Afya, Penford Joel amesema kampeni ya chanjo ya polio itafanyika siku nne hivyo wazazi na walezi wahakikishe watoto wao wao waliochini ya miaka nane wanapata chanjo hiyo.
Amesema kuwa chanjo inamuongezea mtoto kinga ya kupambana ni ugonjwa hivyo watoto watakaopata chanjo hiyo watakuwa salama dhidi ya Polio tofauti na ambao hawatapata ambao watakuwa katika mazingira hatari kuambukizwa ugonjwa huo ambao mpaka sasa hauna tiba.
Amebainisha kuwa ugonjwa huo ukimpata mtoto atapata ulemavu wa kudumu na kusababisha vifo hivyo wananchi wahamasike kuwapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo muhimu.
"Ugonjwa wa Polio umekuwa tishio kwa miaka mingi katika nchi nyingi duniani, na unasababisha kupooza na baadaye vifo. Tunawaomba wananchi mkoa wa Songwe kujitokeza na kuhakikisha watoto wote chini ya miaka nane wanapata chanjo. Kampeni hii ikishapita hawatapata tena hivyo wahakikishe wanatumia siku hizi nne” amesisitiza.
Chanjo hiyo ambayo inatolewa kwa siku nne itaanza Septemba 21 hadi 24, 2023 ambayo itafanyika katika Mkoa wa Songwe, Mbeya, Katavi, Rukwa, Kigoma na Kagera.
Katika Mkoa wa Songwe kampeni hiyo inatarajia kuwafikia na wakuchanja jumla ya watoto 402, 644 ambapo Halmashauri ya Mbozi watoto 180,713 wanatarajiwa kufikiwa, Songwe watoto 53,687, Momba 66,065, Ileje 50,563 huku Halmashauri ya Mji Tunduma ikitarajia kuwafikia watoto 51, 716.
Mbozi
Anuani: 3
Simu: 025-2580272
Simu ya kiganjani:
Barua pepe: ded@mbozidc.go.tz
Hati Miliki 2017 Halmashauri ya Wilaya-Mbozi. Haki zote zimehifadhiwa