Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba amesema kuwa hajutii kufanya kazi katika mkoa wa Songwe kutokana na ushirikiano alioupata kutaka kwa watumishi wa umma na wananchi wakati akiwa mkuu wa mkoa huo huku akiahidi kuwa Songwe itaendelea kubaki moyoni mwake.
Kindamba alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe akihamishiwa mkoa wa Tanga na Rais Samia Suluhu Hassan Februari 26 mwaka huu ambapo nafasi yake ikichukuliwa na Dkt Francis Michael.
Akizungumza wakati wa kukabidhiana ofisi na mkuu wa mkoa huo mpya leo Jumatatu Machi 20, 2023 Kindamba amesema wafanyakazi wengi katika mkoa huo waliishi naye kama ndugu hivyo Songwe itaendelea kubaki moyoni mwake.
"Hamkuwa wafanyakazi tu ila mlikuwa ndugu zangu, mara nyingi familia yangu ilikuwa Dar es Salaam lakini ninyi mlikuwa kama ndugu zangu, kutokana na ushirikiano mliokuwa mnanipa. Sijawahi kujutia kufanya kazi Songwe na itaendelea kubaki moyoni mwangu" amewaambia viongozi na watumishi wa mkoa huo wakati akikabidhi ofisi.
Amebainisha kuwa uahirikiano alioupata ndio uliowezesha kutatua mogogoro ya mara kwa mara katika mji wa Tunduma.
"Tunduma ilikuwa inachemka na migogoro lakini tuliweza kushirikishana na kwa ushirikiano mambo yakawa shwari. Tunduma imepoa kwa sababu ya kushirikishana kutatua migogoro" amesema Kindamba na kuongeza
"Nawashukuru viongozi wenzangu kuanzia ngazi ya mkoa hadi vijiji, tulifanikiwa kwa sababu tulifanya kazi kama timu"
Pia, Kindamba amewataka viongozi na wananchi wa mkoa wa Songwe kupinga ukatili wa kijinsia na vitendo vingine vinavyokwenda kinyume na maadili.
Hata hivyo, Kindamba amemshauri mkuu wa mkoa huyo kuendeleza vipaumbele vilivyokuwa vimewekwa ikiwemo ujenzi wa Bandari Kavu eneo la Mpemba, upanuzi wa barabara ya TANZAM iwe njia nne, mji wa kisasa kata ya Mpemba, stendi ya kisasa ya mkoa na utatuzi wa migogoro ya mipaka.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Songwe (RAS), Happiness Seneda amemshukuru Kindamba kwa namna alivyoishi vizuri na watumishi wa umma wa mkoa huo na kubainisha kuwa Mkuu huyo wa mkoa wa Tanga alikuwa mwalimu kwa wengi wakati akiwa katika mkoa huo.
Mbozi
Anuani: 3
Simu: 025-2580272
Simu ya kiganjani:
Barua pepe: ded@mbozidc.go.tz
Hati Miliki 2017 Halmashauri ya Wilaya-Mbozi. Haki zote zimehifadhiwa