Shirika lisilo la kiserikali la Sanitation and Water Action (SAWA) chini ya ufadhili wa Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) limekabidhi matundu 135 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi yaliyojengwa katika shule mbalimbali za msingi.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo leo Alhamisi Februari 22, 2024, katika shule ya msingi Mlowo
Msimamizi wa Mradi wa SAWA, Mhandisi Wilhelmina Malima amesema lengo la kukabidhi matundu hayo ni kuboresha afya za wanafunzi, usafi wa mazingira, huduma ya vyoo na huduma ya maji ikiwa na lengo la kukuza ufaulu na watoto kufikia ndoto zao, ambapo matundu hayo na miundombinu ya maji vimegharimu zaidi ya Sh600 milioni.
Shughuli zilizofanyika katika Mradi huo ni pamoja na ujenzi wa majengo mapya, uboreshaji wa huduma ya maji, ujenzi wa vifaa vya kunawia mikono, uboreshaji mifumo ya ukusanyaji na uteketezaji taka
Mhandisi Malima amesema kuwa mradi umefanikiwa katika mambo mbalimbali ikiwemo ukarabati wa vyoo, kuimarika kwa tabia za kiafya, upatikanaji wa maji safi, hamasa ya utoaji wa chakula, kuimarika kwa usafi shuleni na ushiriki mkubwa wa jamii.
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Danny Twelve ametoa shukrani za dhati kwa mashirika hayo na kusema kuwa bado upungufu upo wasichoke kutoa misaada hiyo.
"Kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mbozi na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi tunathamini na kuheshimu msaada huu utakao punguza pengo la upungufu wa miundombinu hii ambapo watoto wetu watajisitiri katika mazingira yalio Bora"
Mwakilishi wa Shirika la Watoto Duniani Nyanda za Juu Kusini, Remijius Sungu ametoa shukrani kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kwa ushirikiano na mwitiko mkubwa katika kukamilisha miradi hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbozi, Mhe.George Musyani ameshukuru mashirika hayo kwa kuendelea kuwa na imani na Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kwa kuleta miradi.
Ametoa rai kwa idara zinazohusika na malezi na makuzi ya watoto kuendelea kukumbusha wajibu wao, watoto wazidi kufundishwa namna ya kuitunza na mazingira na miundombinu iliyowekwa katika maeneo yao.
Mbozi
Anuani: 3
Simu: 025-2580272
Simu ya kiganjani:
Barua pepe: ded@mbozidc.go.tz
Hati Miliki 2017 Halmashauri ya Wilaya-Mbozi. Haki zote zimehifadhiwa