Tunduma. Ikiwa imekaribia msimu wa mavuno kwa wakulima wa Mkoa wa Songwe, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk Francis Michael amewataka wakulima kuacha tabia ya kuuza mazao shambani.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya miaka 59 Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Shule ya Sekondari Nyerere mjini Tunduma wilayani Momba leo Jumatano Aprili 26, 2023, Dk Michael amesema kuwa wakulima wakiuza mazao shambani wanajipunja hivyo amewashauri wavune na kuhifadhi kabla ya kuuza ili kupata faida.
"Suala la wakulima kuuza mazao shambani hili ni tatizo maana wanaofanya hivyo wanajipunja, nawashauri wasubiri wavune ndipo wauze" amesema
Mkuu huyo wa mkoa amesema Serikali imetoa ruzuku ya pembejeo za kilimo ili wakulima wanufaike na kilimo.
Kuhusu muungano
Akizungumza kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanziabar, Dk Michael amewataka wananchi na Watanzania wote kudumisha upendo ili muungano huo udumu.
Amesema maadhimisho hayo yanaleta picha ya umuhimu na hamasa ya muungano kwa Tanzania na nchi jirani.
Amesema kuwa mkoa wa Songwe na Halmashauri zake umepiga hatua tangu muungano katika sekta mbalimbali ikiwemo ellimu, kilimo, huduma za afya na miundombinu.
Uzinduzi wa miradi ya maendeleo
Kabla ya maadhimisho hayo, Mkoa wa Songwe na hamlashauri zake umefanya shughuli mbalimbali ikiwa ni alama ya maadhimisho hayo.
Miongoni mwa shughuli zilizofanyika katika mkoa huo ni pamoja na kutembelea, kukagua na kuzindua miradi ya maendele ikiwemo miradi ya maji na shule.
Miongoni mwa miradi iliyozinduliwa ni pamoja na mradi wa maji wa Nselewa-Mlowo ambao ulizinduliwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso jana.
Mradi huo utahudumia zaidi ya wananchi 15,000 wa kata ya Vwawa na Mlowo wilayani Mbozi.
Leo wakati wa maadhimisho hayo, Dk Michael amezindua mradi wa shule ya Msingi Msongwa iliyojengwa kwa gharama ya Sh250 milioni fedha za programu ya lipa kulingana na matokeo- EP4R.
Kuimarisha ujirani mwema
Ili kuimarisha uhusiano na ujirani mwema kati ya Mkoa wa Songwe na nchi jirani, Dk Michael amesema maadhimisho hayo wamealika baadhi ya wananchi kutoka nchi jirani ya Zambia ambapo timu ya mpira imeshiriki katika michezo pamoja na timu zingine za mkoa huo.
"Sherehe hii ni kubwa ndio maana tumealika tumu kutoka Zambia zanashiriki michezo kwa sababu suala la muungano ni suala la kimataifa"
"Tumeungana Tanzania lakini bado kuna nia kubwa ya kuungana nchi za Afrika tupate Afrika moja, tunafanyaje hivyo ni kuzihamasisha nchi jirani zione umuhimu na kupata hamasa muungano" amesema mkuu huyo wa mkoa.
RAS ahamasisha mazoezi kujenga afya
Akizungumza baada ya mazoezi ya mbio jogging ambayo ni miongoni mwa shughuli zilizopamba maadhimisho hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Happiness Seneda amewataka wananchi kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujenga afya na kujiepusha na magonjwa yasiyoambukiza.
Katibu Tawala huyo amesema ili kufanha kazi za maendeleo ni lazima kuwa timamu kiafya hivyo mazoezi ni nyenzo muhimu katika kujemga afya.
"Nawaomba wote mlioshiriki mazoezi haya msiishie hapa, mazoezi ni muhimu kujenga afya na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza" amesema RAS huyo ambaye ameongoza jogging iliyoanzia Kilimanjaro mjini Tunduma hadi viwanja vya Shule ya Sekondari Nyerere mjini humo.
"Ili ufanye kazi vizuri lazima uwe na afya nzuri na afya nzuri inajengwa na mazoezi hivyo nawaomba mfanye mazoezi" amesisitiza.
Usiku wa mungano
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Momba ambaye ndiye mwenyeji, Fakih Lulandala amesema maadhimisho hayo yatahitimishwa leo usiku kwwnye tukio maalumu ambalo limeandaliwa litakalowakutanisha wadau mbalimbali wa kutoka mkoa huo.
Lulandala amesema wanayofuraha maadhimisho hayo kufanyika katika wilaya yake kimkoa ambapo pia amewakaribisha wadau mbalimbali katika tafeija hiyo itakayofanyika leo usiku ambayo imepewa jina la Usiku wa muungano.
Katika tukio hilo mgani rasmi atakuwa Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamis Hamza
Mbozi
Anuani: 3
Simu: 025-2580272
Simu ya kiganjani:
Barua pepe: ded@mbozidc.go.tz
Hati Miliki 2017 Halmashauri ya Wilaya-Mbozi. Haki zote zimehifadhiwa