Wauguzi wa Mkoa wa Songwe wametakiwa kuendelea kutoa huduma bora na salama kwa kuheshimu utu wa mtu bila ubaguzi.
Wito huo umetolewa na leo Ijumaa Mei 31, 2024 na Katibu Tawala Mkoa wa Songwe Bi. Happiness Seneda wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani ambapo kimkoa yamefanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Bi. Seneda amesema kuwa jamii inatambua kazi kubwa inayofanywa na wauguzi.
"Ninafahamu kuwa wauguzi wengi wanafanya kazi zao vizuri kwa kuzingatia maadili na msingi bora ya taaluma yao, ingawa wapo wachache ambao wanataka kuichafua taaluma" amedokeza na kuongeza;
"Natoa wito kwa viongozi, wauguzi hao wanaokwenda kinyume na maadili ya taaluma yenu msiwafumbie macho, bali mfanye jitihada za kuwabaini na kuwarekebisha. Mamlaka zao za nidhamu ziwachukulie na hatua za kimaadili kwa kuwafikisha kwenye baraza lenu"
"Nimesikia changamoto mlizowasilisha ambazo kwa namna moja au nyingine zinachangia kupunguza ubora wa utendaji kazi zenu ikiwa ni pamoja na upungufu wa wauguzi katika vituo vya kutolea huduma, hili ni tatizo la nchi nzima pamoja na tatizo hili Rais wetu anaendelea kutoa ajira kwa awamu tofauti"
Kuhusu suala la waajiri kutowaruhusu wauguzi kushiriki makongamano ya kitaaluma kwa kushindwa kuwagharamia, Katibu Tawala huyo amewaagiza wakurugenzi kutenga fungu la kuwawezesha wauguzi hao kushiriki.
Akizungumzia changamoto ya wauguzi kutopata posho ya sare ya kazi, amesema kuwa kuwa ni takwa la kimuundo hivyo ni wajibu wa waajiri wote kuhakikisha wauguzi wanapatiwa posho ya sare za kazi.
Siku ya Wauguzi duniani huadhimishwa kwa heshima ya Wauguzi na wafanyakazi wa afya ulimwenguni kote.
Siku hii ilitengenezwa kwa heshima ya Florence Nightingale, ambaye alikuwa muuguzi maarufu uingereza na manzilishi wa taaluma ya uuguzi wa kisasa
Mbozi
Anuani: 3
Simu: 025-2580272
Simu ya kiganjani:
Barua pepe: ded@mbozidc.go.tz
Hati Miliki 2017 Halmashauri ya Wilaya-Mbozi. Haki zote zimehifadhiwa