Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema Tanzania ina uhitaji wa viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo kwa kuwa zaidi ya asilimia 65 wamejiajiri katika kilimo.
Kigahe amebainisha hayo leo Jumatano Agosti 10, 2023 wakati wa ziara yake ya kutembelea Kiwanda cha Kahawa cha GDM na Kiwanda cha Ilasi Sembe katika Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe.
Amesema kuwa kama mazao yataongezewa thamani itakuwa tija kwa wakulima na mapato yataongezeka.
"Viwanda hivi vinavyoongeza thamani mazao ya kilimo vitasaidia mazao yetu yaongezewe thamani ili kuleta tija na mapato kwa wakulima" ameeleza
Naibu Waziri huyo ambaye alikuwa anahitimisha ziara yake ya Siku mbili mkoani Songwe amesema changamoto inayozikumba nchi nyingi za Afrika ni kuzalisha bidhaa ambazo hawazitumii.
Ametoa wito kwa viwanda ambavyo vinategemea malighafi kutoka kwa wakulima kuwasaidia pembejeo na mbegu ili wazalishe kwa tija hali itakayosaidia viwanda kupata malighafi.
Hata hivyo, Kigahe ameipongeza Mkoa wa Songwe na Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kwa usimamizi mzuri wa minada ya kahawa.
"Niwapongeze Mkoa na Halmashauri (Mbozi) kwa kuhakikisha minada ya kahawa inafanyika hapa Mbozi zamani mlikuwa mnategemea kule Moshi na Arusha ambapo inakuwa gharama kusafirisha" amesema
Amesema kazi ya Wizara hiyo ni kuweka mazingira wezeshi ikiwa ni mojawapo ya mkakati wa kuboresha uwekezaji.
"Tumekubaliana kuanzisha eneo huru la biashara kama nchi za Afrika kuuziana sisi kama sisi. Tumeshaanza kufanyiana hivyo na sisi Tanzania tunapata fursa kubwa kuwauzia kwa bei nzuri" amesema
Naibu Waziri huyo amehitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Songwe ambapo pamoja na mambo mengine alitembelea Kituo cha Pamoja cha Forodha Tunduma, kutembelea Kiwanda cha Kahawa cha GDM, Kiwanda cha Ilasi Sembe na kuhitimisha kwa kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa mkoa wa Songwe
Mbozi
Anuani: 3
Simu: 025-2580272
Simu ya kiganjani:
Barua pepe: ded@mbozidc.go.tz
Hati Miliki 2017 Halmashauri ya Wilaya-Mbozi. Haki zote zimehifadhiwa