Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Umeme Vijijini, Mhandisi Hassan Said amewataka wananchi wa Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe kutunza na kulinda miundombinu ya umeme huku akiwataka kuhakikisha wanatumia umeme kwa usalama.
Mkurugenzi huyo ametoa rai hiyo leo Jumamosi Agosti 5, 2023 akiwa katika Kata ya Bara na Isansa Wilayani Mbozi wakati wa ziara ya kuzindua mradi wa nishati mzunguko wa pili katika kata hizo.
Amesema "Rai yangu mtunze na kulinda miundombinu hii na mhakikishe kuwa matumizi ya umeme yanatumika salama hasa kwa vijana wadogo. Tuepuke kukaa chini ya transifoma" amesisitiza
Mkurugenzi huyo amewasisitiza wananchi ambao bado hawajaomba umeme waombe ili wawekewe nishati hiyo.
Amesema kuwa kuna mradi mpya ambao unatarajiwa kuanza hivi karibuni katika Mkoa wa Songwe ambapo vitongoji 151 vitasambaziwa umeme kati ya hivyo 68 kutoka Wilaya ya Mbozi sawa na asilimia 45 ya mradi huo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Umeme Vijijini, Janeth Mbene amesema kuwa Serikali imeweka historia kupeleka umeme vijijini ikiwemo katika kata ya Bara na Isansa Wilayani Mbozi ambayo ilikuwa haijapata umeme tangu uhuru.
"Kwa bahati nzuri fedha za kuendesha nishati vijijini zipo mama yetu (Rais Samia) anahakikisha kuwa hela haikomi kutokana na vyanzo mbalimbali ambavyo vipo serikalini. Lengo la kuleta umeme ni kuchochea uchumi" amesema
Naye Mkurugenzi wa Tanesco Kanda ya Kusini Magharibi, Mhandisi Sotko Nombo amewatahadharisha wananchi kutokufanya shughuli za kijamii chini ya laini kubwa ya kupitisha umeme.
Mhandisi Nombo amewataka wananchi wa kata hiyo kuomba kuunganishiwa umeme ambapo gharama yake ni Sh27, 000 kwa maeneo hayo ya vijijini.
Mbunge wa Mbozi, Ranwelo Mwanisongole amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza wajibu wake wa kuwapelekea wananchi umeme.
Mbozi
Anuani: 3
Simu: 025-2580272
Simu ya kiganjani:
Barua pepe: ded@mbozidc.go.tz
Hati Miliki 2017 Halmashauri ya Wilaya-Mbozi. Haki zote zimehifadhiwa