MBOZI. Wanawake wametakiwa kupaza sauti ili kupinga vitendo vya ukatili vinavyoefanywa katika jamii zao.
Pia, wametakiwa kuungana katika vikundi ili kunufaika na fursa zinazojitokeza katika maeneo yao.
Rai hiyo imetolewa leo Jumatano Machi 8, 2023 na Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Mkoa wa Songwe, mama Tunu Pinda ambeye ni Mke wa Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda.
Mgeni huyo rasmi amesema vipo vikwazo ambavyo vimekuwa vikikwamisha wanawake kujikwamua kiuchumi ikiwamo mila, kutokuthubutu na kukata tamaa.
Amewataka kutumia fursa ya mikopo inayotolewa na Serikali ili kuwawezesha kuinuka kiuchumi.
"Kina mama kopeni msiogope maadam mnarudisha, kutumia fursa zinazopatikana katika maeneo yetu ili kuanzisha viwanda" amesema
Amesema Serikali ipo tayari kuwapa wanawake mikopo nchini kupitia asilimia 10 za mapato ya halmashauri hivyo wanawake watumie fursa hiyo.
"Tuungane pamoja na kufanya kazi kwa bidii na kufikiria nje ya boksi, kila fursa inayotokea mwanamke awe mbele ili afanikiwe" ameshauri mgeni huyo rasmi
Amesema kutokana na kutokuwepo usawa wa kijinsia, bado wanawake wanashindwa kujikwamua kutokana na kukandamizwa hivyo amewataka kuungana kupinga mila na tamaduni katika jamii.
Amesema ni wakati wa wanawake kuungana na kupambana kupinga ukatili wa kijinsia.
"Tupambane na kupinga ukatili wa kijinsia. Tuhakikishe vitendo vya udhalilishaji kutokomea nchini" amesema
Pia, amewataka wanawake kuzingatia lishe ili kutokomeza udumavu kwa watoto.
"Suala la lishe ni muhimu kwa watoto wetu, elimu itolewe kuanzia kwa mama anayetarajia kupata ujauzito na aliye na ujauzito kwa kila kaya ili kupata watoto wenye afya bora" amesema
Mbozi
Anuani: 3
Simu: 025-2580272
Simu ya kiganjani:
Barua pepe: ded@mbozidc.go.tz
Hati Miliki 2017 Halmashauri ya Wilaya-Mbozi. Haki zote zimehifadhiwa