Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbozi, ndugu Mbwana Kambwangwa amewapongeza wananchi wa Kata ya Itumpi Wilaya ya Mbozi kwa kuchangia zaidi ya tani 35 za chakula kwaajili ya kuwezesha watoto wao kupata chakula shuleni katika Kata hiyo.
Ndugu Kambangwa ametoa pongezi hiyo wakati wa kikao kazi cha kuzungumza na watumishi wa Serikali wa Kata ya Itumpi chenye lengo la kufahamiana kilichofanyika Mei 18, 2024.
Amesema kuwa hiyo imeweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kila mzazi mwenye mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari anachangia chakula wakati wa mavuno ili kutatua changamoto ya ukosefu wa chakula kwa wanafunzi.
"Niwapongeze sana kwa kuweka mikakati madhubuti katika zoezi la kukusanya chakula katika shule zenu tano za msingi na moja ya sekondari na mpaka sasa mna zaidi ya tani 35 za chakula, hii sio mchezo hongereni sana walimu, mheshimiwa diwani na kamati ya maendeleo ya kata" amesema
"Hii imeonyesha jinsi gani wote mnaongea lugha moja. Maharage mmekusanya tani nne mmejitahidi sana. Na hili tunalibeba kama mfano katika maeneo mengine. Utolewaji wa chakula mashuleni ni moja ya kiashiria cha shule salama"
Amewataka wale waliopewa dhamani ya kusimamia zoezi la chakula mashuleni kuwa waadilifu na kuzingatia weledi katika kusimamia matumizi ya vyakula na fedha zilizochangwa.
Pia, Katibu Tawala huyo amewasisistiza watumishi hao kuzingatia malezi kwa watoto na watu wazima ikiwa ni pamija na kuchukua tahadhari ya mambo ya ulawiti, ubakaji na ukatili.
Kata ya Itumpi imeweka utaratibu wa wazazi kuchangia chakula cha wanafunzi wakati wa mavuno kitakachohifadhiwa na kutumika mpaka msimu unaofuata
Mbozi
Anuani: 3
Simu: 025-2580272
Simu ya kiganjani:
Barua pepe: ded@mbozidc.go.tz
Hati Miliki 2017 Halmashauri ya Wilaya-Mbozi. Haki zote zimehifadhiwa