Wananchi wa mji wa Vwawa na Mlowo wilayani Mbozi wametakiwa kutoa maoni yatakayosaidia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vwawa-Mlowo (WSSA) kutoa huduma bora ya maji.
Pia, wametakiwa kulipia bili za huduma ya maji kwa wakati na kuhifadhi miundombinu ya maji katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa leo Alhamisi Agosti 17, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Esther Mahawe akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk Francis Michael wakati akifungua mkutano wa taftishi kuhusu ombi la kurekebisha bei za huduma za maji safi na usafi wa mazingira za Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vwawa-Mlowo (WSSA) uliondaliwa na Ewura unaoendelea mjini Vwawa.
DC Mahawe amesema "Wananchi wana haki ya kutoa maoni ya huduma wanayoipata na wana haki ya kupata huduma kwa wakati na ubora hivyo nawaomba mtoe maoni yatakayosaidia mamlaka kutoa huduma bora na changamoto mnazokutana nazo"
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Mhandisi Mkuu Violet Iram amesema kuwa mapendekezo ya marekebisho hayo yaliyopendekekezwa na WSSA yanalenga kuiwezesha Mamlaka kutekeleza shughuli zilizoainisha katika mpango biashara wake kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2023/24 na 2025/26.
"Bei zinazopendekezwa zitasaidia shirika kurejesha gharama za uendeshaji na matengenezo pamoja na kukidhi baadhi ya gharama za ukarabati, uingizwaji na uwekeaji mpya na hivyo kutoa huduma ya maji ya kutosha, safi na salama katika maeneo ya huduma Vwawa-Mlowo" amebainisha
Mkurugenzi Mtendaji wa WSSA, Mhandisi Clavery Casmir amesema kuwa mabadiliko hayo ya bei za maji yatawasaidia kukamilisha miradi mbalimbali inayotekelezwa ili kuboresha usambazaji wa maji kwa wananchi wa Vwawa na Mlowo.
Amesema Mamlaka hiyo pia ina mkakati wa kutoa maji mto Momba ambapo mradi huo utasaidia kutatua adha ya maji kwa mji wa Tunduma, Vwawa na Mlowo.
Mbozi
Anuani: 3
Simu: 025-2580272
Simu ya kiganjani:
Barua pepe: ded@mbozidc.go.tz
Hati Miliki 2017 Halmashauri ya Wilaya-Mbozi. Haki zote zimehifadhiwa