Mbozi. Uongozi wa Shule ya Msingi Mwenge kitengo Cha wanafunzi wenye mahitaji maalumu iliyopo wilayani Mbozi umeishukuru Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuwepo wanafunzi wenye ulemavu na kuwapa fursa ya kupata elimu.
Shukrani hizo zimetolewa leo Jumanne Machi 21, 2023 wakati wa ziara ya wakuu wa idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi (CMT) katika shule hiyo.
Akisoma taarifa ya kitengo hicho mwalimu wa wanafunzi wasioona, Revina Kayombo amesema kuwa wanaishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kwa kuwapelekea kitengo cha iposa kwa wanafunzi wenye ulemavu wa akili ambacho kitengo hicho kinawasaidia kujifunza masuala ya ufundi baada ya kumaliza elimu ya msingi kama hawajachaguliwa kujiunga na sekondari.
"Wanafunzi hawa wanaweza sana masuala ya ufundi na michezo na wanaweza kufanya vizuri zaidi"
Mwalimu huyo ametaja changamoto wanazokutana nazo katika kitengo hicho ikiwemo ukosefu wa kisima cha maji ya kudumu, choo maalumu kwa wanafunzi wenye ulemavu wa viungo, uzio wa bweni la kike.
Changamoto zingine alizozitaja mwalimu Kayombo ni pamoja na uhaba wa vyumba vya madarasa, bwalo la chakula, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, upungufu wa walimu, vifaa vya michezo, maktaba, samani na uwanja wa michezo.
Uongozi huo umetoa mapendekezo ya kuwepo matangazo maalumu kuhusu watu waenye mahitaji maalumu ili kuwafikia kwa urahisi.
Pia, umeomba mazingira ya shule kuboreshwa kulingana na mahitaji ya watoto wenye ulemavu, serikali kuajiri mlinzi, mpishi na matroni wenye uelewa na elimu maalumu.
Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha elimu maalumu shuleni hapo, Eden Ngogo ametaja mchakato wa kuwapata watoto hao kuwa ni pamoja na kuzunguka majumbani kuwatafuta, kutoa elimu katika nyumba za ibada, kupata taarifa kutoka kwa watu mbalimbali.
Mkuu huyo ambaye pia ni mlemavu wa macho ameiomba Serikali kuanzisha sekondari ya mkoa ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu ili kuzidi kuwasaidia watoto hao kuyafikia malengo yao.
Mwalimu wa wanafunzi wenye ulemavu wa akili, Alois Chacha amesema kuwa kuna watoto ambao wanamatatizo ya akili lakini wanamudu suala la michezo.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Oscar Mgani amewapongeza walimu wa shule hiyo hasa kitengo cha elimu maalumu kwa kuwafundisha na kuwahudumia wanafunzi hao.
Mbozi
Anuani: 3
Simu: 025-2580272
Simu ya kiganjani:
Barua pepe: ded@mbozidc.go.tz
Hati Miliki 2017 Halmashauri ya Wilaya-Mbozi. Haki zote zimehifadhiwa