Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amewataka watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Songwe kuwafwata wafanyabiashara katika maeneo yao ili kuwapa elimu na kujadiliana namna ya kulipa kodi badala ya kuwasubiria wafanyabiashara kuja ofisini.
Kigahe ameyoa agizo hilo leo Jumatano Agosti 10, 2023 wakati wa mkutano wake na baadhi ya wafanyabiashara wa mkoani huo mjini Vwawa.
"Mimi nadhani muende katika maeneo yao ya biashara badala ya kuwasubiri wafanyabiashara kuja ofisini" amesema na kuongeza;
"Tutoke tukawaelimishe watu. Naona mkienda katika maeneo ya wafanyabiashara mtatoa elimu na kukubaliana namna ya kupanga kodi na utaratibu huo utakuwa na matokeo chanya" amesema
Akizungumza katika mkutano huo Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Songwe, Aderick Alphonce amesema kuwa wamepokea maagizo hayo na wanakwenda kuyafanyia kazi.
"Kuanzia sasa tutakuwa tunakuja katika biashara zenu kutoa elimu na msiwaogope maofisa wa TRA" ameahidi Kaimu Meneja huyo wa TRA.
Akizungumzia kuhusu changamoto ya Barabara ya Tanzam, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbozi (DAS), Mbwana Kambangwa amesema kuwa barabara hiyo imeanza ujenzi wake ambapo ikikamilika itatatua changamoto ya usafirishaji.
"Changamoto ya barabara kutoka Igawa mkoa wa Mbeya mpaka Tunduma mkoa wa Songwe inajengwa kwa thamani ya Sh1.1 trilioni na itajengwa kwa kiwango cha kimataifa. Tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha hili" amesema Katibu Tawala huyo.
Baadhi ya wafanyabiashara wameiomba Serikali kupitia halmashauri kupunguza kodi na tozo mbalimbali ili kuwafanya wafanyabiashara hao kulipa kodi.
Pia, wameiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoa elimu ya mlipa kodi pamoja na kujenga urafiki na wafanyabiashara hao.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara ndogondogo maarufu machinga Mkoa wa Songwe, Kelvin Kyando amesema kuwa kumekuwa na kodi zisizo na usawa ambazo zinawakimbiza wafanyabiashara wengi.
"TRA wawe na tabia ya kutoa elimu kwa wafanyabiashara waweze kulipa kodi kwa urahisi. Pia watengeneze mazingira rafiki kwa wafanyabiashara" amesema Kyando
Naye mfanyabiashara Georgina Chaula ameiomba Halmashauri kupunguza kodi kwa wafanyabiashara wadogo.
Kwa upande wake mfanyabiashara wa mchele amesema kuwa hakuna soko maalumu la mchele katika mji wa Vwawa pamoja na pumba hivyo kuomba kutengewe eneo maalumu.
Naibu Waziri Kigahe yupo kwenye ziara ya siku mbili katika Mkoa wa Songwe ambapo jana alitembelea Kituo cha Pamoja cha Forodha cha Mpaka Tunduma katika mpaka wa Tanzania na Zambia
Mbozi
Anuani: 3
Simu: 025-2580272
Simu ya kiganjani:
Barua pepe: ded@mbozidc.go.tz
Hati Miliki 2017 Halmashauri ya Wilaya-Mbozi. Haki zote zimehifadhiwa