MBOZI. Kamati ya Uchumi, Fedha na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi imetoa wiki mbili kwa kijiji cha Shilanga kata ya Ihanda kupiga hatua ukamilishaji wa zahanati ya ya kijiji hicho baada ya kupokea Sh50 milioni kwaajili ya ukamilishaji lakini bado hawajaanza kuzifanyia kazi.
Agizo hilo limetolewa leo Jumatatu Aprili 3, 2023 na Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbozi, George Musyani wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali katika halmashauri hiyo.
Musyani amesema kuwa kijiji kilishapokea Sh50 milioni tangu mwezi Februari mwaka huu lakini mpaka sasa hakijaanza ujenzi.
Amesema kuwa kama wiki mbili zitapita bila utekelezaji wa agizo hilo, fedha hizo zitahamishiwa kwenye vijiji vingine ambavyo vina uhitaji.
"Baada ya sisi kuondoka mkae kama kijiji mjadili jinsi gani mtakamilisha kazi hii, baada ya wiki mbili tutakuja kukagua kuwa mmefikia wapi na kama bado mtakuwa mnasuasua fedha hizo tutazihamisha na kuzipeleka katika vijiji vinavyohitaji" amesisitiza mwenyekiti huyo wa halmashauri.
Amesema " Kila kitu mnacho, fedha mnazo sio kusema kuwa kuna kitu mnakitafuta ni mchakato tu unasuasua kuanza, kwa kusuasua huku inaonyesha nyie hamna uhitaji"
Mwenyekiti huyo amesema kuwa ameshangazwa na taarifa za kuwa wananchi hawahudhurii kwenye mikutano ya kijiji kutokana na kokosekana kwa posho.
Kwa upande wake Diwani wa Viti Maalum Tarafa ya Vwawa, Neema Nzowa amewataka wananchi wa kijiji hicho kuhudhuria mikutano ya kijiji ili kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Diwani huyo amesema kuwa inawezekana wananchi hawahudhurii mikutano ya vijiji kutokana na kusitishwa kwa posho zilizokuwa zikitolewa kipindi cha nyuma.
Mkazi wa kijiji hicho, Adam Senka amewataka wananchi kuwa wafuailiaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili itekelezwe kwa wakati.
Ujenzi wa zahanati hiyo ambayo itawahuumia wananchi zaidi ya 400 ulianza mwaka 2011.
Kwa sasa wananchi wa kijiji hicho wanalazimika kwenda katika Zahanati ya Ihanda au Hospitali ya Wilaya ya Mbozi kupata huduma za afya.
Mbozi
Anuani: 3
Simu: 025-2580272
Simu ya kiganjani:
Barua pepe: ded@mbozidc.go.tz
Hati Miliki 2017 Halmashauri ya Wilaya-Mbozi. Haki zote zimehifadhiwa